
Simba SC jana ilitoka sare ya kufungana bao
1-1 na Tusker ya Kenya katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Mapinduzi
kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Kwa matokeo hayo, Tusker inaendelea kuongoza Kundi
A, kwa piointi zake tatu sawa na Simba, lakini mabingwa hao wa Kenya wana
wastani mzuri zaidi wa mabao.
Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimekwishafungana
bao 1-1, Simba wakitangulia kupata bao dakika ya 18 mfungaji Haruna Moshi
Shaaban, maarufu kama Boban au Balotelli wa Bongo kabla ya Tusker kusawazisha
dakika ya 39, mfungaji Khalid Aucho.
Boban alifunga bao tamu sana kwa ufundi wa hali juu
akiwa amedhibitiwa na beki ngongoti wa Tusker, Joseph Shikokoti na kuirukia
pasi ya Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kuitumbukiza nyavuni.
Baada ya kufunga bao hilo, Boban aliangukia mkono
na kuumia, hivyo hakushangilia bao lake na moja kwa moja alianza kutibiwa na
Daktari Cossmas Kapinga wa Simba.
Baada ya bao hilo, Simba iliongeza mashambulizi
langoni mwa Tusker na Boban alikaribia kufunga tena dakika ya 30 kama si shuti
lake kutoka nje sentimita chache.
Aucho alifunga bao lake akiunganisha krosi ya
Jeremiah Bright kutoka upande wa kushoto wa Uwanja.
Baada ya hapo, timu zilianza kushambuliana kwa zamu
hadi refa Ramadhani Kibo alipopuliza kipyenga cha kuhitimisha ngwe ya kwanza.
Kipindi cha pili timu zote zilirudi vizuri na
kucheza kwa umakini wa hali ya juu, jambo ambalo lilisababisha dakika 90
zimalizike zikiwa zimefungana 1-1.
Katika mchezo huo, kikosi cha Simba kilikuwa; William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema, Shomary
Kapombe, Komabil Keita, Jonas Mkude, Haroun Athumani/Mussa Mudde 75, Mwinyi
Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi na Ramadhan Chombo ‘Redondo’/Edward
Christopher dk 52.
Tusker FC; Samuel Odhiambo, Luke
Ochieng, Jeremiah Bright/Humphrey Okoth, Mark Odhiambo, Joseph Shikokoti,
Khalid Aucho, Edwin Manono/Benson Amanda, Justin Monda, Ismail Dunga/Michael
Olunga, Jesse Were na Robert Omonuk.
Katika mchezo uliotangulia, Jamhuri ilishinda mabao
2-1 dhidi ya Bandari kwenye Uwanja wa Mao Dze Tung. Mabao ya Jamhuri yalifungwa
na Fahad Abdallah Athumani dakika ya 25 na Ally Bilal dakika ya 67, wakati la
Bandari lilifungwa na Faudhi Ally dakika ya tano.
0 comments:
Post a Comment