Udinese na msimu mpya wa Serie A 2012-13
Mpaka sasa mashabiki wa klabu ya soka ya Udinese ya nchini Italia au waweza kuwaita Pundamilia wadogo(Zebrette) au Bianconerri(nyeupe na nyeusi) kutokana na jezi zao kuwa na rangi nyeusi na nyeupe hawaamini kama timu yao imeweza kumaliza katika nafasi za juu za ligi kuu ya soka nchini Italia maarufu kama serie A na pia kupata nafasi ya kushiriki hatua za awali za michuano ya klabu bingwa barani ulaya maarufu kama(UEFA Champions League) kwa msimu wa mwaka 2012-13.
Wakishika nafasi ya tatu nyuma ya vilabu vikongwe Italia vikiongozwa na bingwa Juventus pamoja na makamu bingwa AC Milan,Udinese waliendelea kuwashangaza wapenda kabungu wengi ulimwenguni pamoja na mashabiki wake kwani pamoja na timu hiyo kuwa na historia ya kuondokewa na nyota wake mara kwa mara kwa kujiunga na vilabu vikubwa ambavyo kwa kiasi kikubwa vimeifanya klabu ya Udinese kuwa kama chimbo au soko la kununua nyota wanaowika katika klabu hiyo ya Friuli-Venezia nchini Italia,Udinese walivishinda vilabu kama Inter Milan,Lazio,AS Roma na Napoli katika mbio za kuwania nafasi ya kucheza michuano ya klabu bingwa ulaya msimu wa 2012-13.
Hakuna asiyejua kuwa klabu ya Udinese imewatoa nyota wengi mno ambao waling’aa sana wakiwa na klau hiyo.Wachezaji wengi bora kama Nestor Sensini, Oliver Bierhoff, Marcio Amoroso, Vincenzo Iaquinta, David Pizarro, Martin Jørgensen na bila kuwasahau Sulley Muntari, Fabio Quagliarella, Antonio Di Natale, Felipe, Cristián Zapata, Simon Pepe,Gökhan Inler, Alexis Sánchez na wengine wengi wakipitia klabu hii na kuifanya kuwa moja kati ya vilabu vikubwa na vyenye nguvu nchini Italia.
Msimu uliopita ulikuwa wa kampeni nzito kwa kocha Francesco Guidollin na timu yake ya Udinese Calcio mana ulihusisha ushindani toka kwa vilabu vikubwa kwa maana kama Juventus,Inter Milan,Napoli,Roma bila kusahau vilabu vingine shiriki katika serie A kama Genoa,Chievo,Atalanta,Parma,Siena na vilabu vyote shiriki katika serie A msimu uliopita 2012.
Lakini walikuwa ni pundamilia hao wadogo ambapo ilibaki kidogo tu nao waandike historia ya kuutwaa ubingwa wa serie A msimu uliopita kama kusingekuwa na umakini kwa vilabu vya Juventus na AC Milan.
Msimu huu tena kama ilivyoada tutawakosa baadhi ya nyota kunako klabu hiyo kwani familia ya Pozzo ambayo ndiyo wamiliki wa klabu hiyo wameendelea na utaratibu wao wa kuuza nyota na kuingiza nyota wapya katika klabu hiyo.Nyota kama Kwadwo Asamoah,Mauricio Isla,Antonio Floro Flores,Gabriel Toje na Damiano Ferronetti pamoja na Samir Handanovic hawataonekana katika viwanja vya Friuli kutokana na kuuzwa katika vilabu vya Juve,Inter na wengine mikataba yao kuisha au kupelekwa kwa mkopo katika vilabu vingine kama Granada.
Pia kukiwa na tetesi za kuondoka kwa baadhi ya nyota kama Pablo Armero na Danilo,klabu ya Udinese kwa mshangao wa wengi haionekani kutetereka na ndiyo kwanza maisha ndani ya Friuri-Venezia Giulia yakiendelea kama kawaida.
Embu tuiangalie Udinese kiufundi,Je kuondoka kwa nyota kama Handanovic,Kwadwo Asamoah na Isla kunaweza kuigharimu Udinese msimu huu wa 2012-13?tuanze na nafasi ya golikipa
Nafasi ya Golikipa.
Hakuna shaka kuwa Samir Handanovic ni mmoja wa makipa bora sana kwa sasa barani ulaya. Na nawapongeza Inter Milan kwa kumchukua golikipa huyu kwani ataongeza ‘clean sheet’au uimara katika sehemu ya ulinzi wa Inter Milan msimu ujao.Kuondoka kwake Udinese kunatoa nafasi ya kurudi kwa kipa Zelijko Brkic aliyekuwa kwa mkopo kunako klabu ya Siena.Brkic alikuwa na msimu mzuri sana pale Siena kwani aliweza kuiongoza vyema ngome ya Siena ikiwa na mabeki Roberto Vitiello, Cristiano Del Groso na Claudio Terzi.Hivyo kurudi kwa Brkic kunaondoa mashaka kidogo kwa nafasi ya golikipa katika klabu ya Udinese.
Nafasi ya ulinzi (mabeki wa kati na pembeni).
Kwa bahati nzuri sehemu hii nyeti haijaguswa kabisa.Tumeshuhudia kuondoka kwa Asamoah,Isla na wengineo ambao wanacheza katika nafasi za viungo na ushambuliaji lakini si kwa nafasi ya ulinzi ambayo ilifanya vizuri sana msimu uliopita na kuna kila dalili safu ya ulinzi ya Udinese ya msimu uliopita ikawepo tena msimu huu.Hapa nawazungumzia Mehdi Benatia,Danilo na Maurizo Domizzi ambao naamini watakuwepo katika klabu hiyo msimu ujao.Mabeki hao watasaidiwa naAndrea Coda,Joel Ekstrand mchezaji mpya Thomas Hertaux ambaye ametokea klabu ya Caen ya nchini Ufaransa.Hivyo kwa kiasi kikubwa sehemu ya ulinzi ya Udinese inaonekana kuwa na usalama mkubwa.
Nafasi ya mabeki wa pembeni (ambao hucheza
kama ma ‘wing backs’).
Sehemu hii ilikuwa na umuhimu mkubwa sana
katika mtindo au staili ya uchezaji ya klabu ya Udinese.Ikiongozwa na mserbia
Dusan Basta pamoja na Pablo Armero hakika Udinese walikuwa hatari sana msimu
uliopita.Kama Armero hataondoka, basi Udinese watatisha sana wakiendelea kuwa
na hawa ma ‘wing backs’Basta na Armero,Sehemu hii imeongezewa nguvu na ujio wa
Marco Faraoni toka klabu ya Inter Milan na mfaransa Jean Alain Fanchome bila
kumshau Giovanni Pasquale ambaye alikuwa na msimu bora kabisa wa serie A wa
mwaka jana.
Nafasi ya kiungo.
Hakuna mpenda kabumbu asiyejua unyeti wa
idara hii kwani ndiyo inayotufanya wapenzi wengi wa soka kupenda kuangalia
mpira.Hapa ndipo tuliwaona na tunaendelea kuwaona kina
Zidane,Vieira,Wilshere,Redondo,Effenberg,Pirlo,Iniesta,Scholes,Xavi nk.Uwepo wa
kiungo mpambanaji Giampiero Pinzi na kuja kwa kiungo mchapakazi mwingine
Willians maarufu kama(Pitbull) utazidi kuimarisha klabu ya Udinese hasa katika
sehemu ya kiungo.Ni nafasi pia kwa mwafrika Emanuel Badu kuweza kung’aa pamoja na chipukizi wengine kama Robert
Pereyra na Christian Battochio kuweza kufanya vizuri kwa msimu unaokuja wa ligi.
Trequartista au unaweza kumwita mshambuliaji wa pili.Ni eneo la kujidai ambalo vijana wengi wa mjini wanapenda kuliita ‘shimoni’ ambalo kwa kiasi kikuubwa ndilo tumepata kuwashuhudia wachezaji kama Del Piero,Baggio,Totti na sasa tunamshuhudia Cassano.Pia wachezaji kama Messi,Thomas Muller wakijidai mno katika sehemu hiyo maarufu kama Trequartista.Ni eneo ambalo walipata nalo shida mno Udinese msimu uliopita kwani hakupatikana mtu sahihi katika eneo hili ambaye angekuwa akicheza sambamba na mshambuliaji Antonio Di Natale.
Lakini kwa msimu huu mpya wa ligi, mchezaji Diego Fabbrini ameonekana kufiti vizuri sana katika eneo hilo hasa katika mechi za maandalizi ya msimu mpya unaokuja (pre-season).Uwepo wa Fabbrini na ujio wa nyota mpya Mbrazili Maicosuel toka klabu ya Hoffenheim(Ujerumani) utaongeza nguvu katika eneo hilo na sehemu ya ushambuliaji kwa ujumla.
Nafasi ya ushambuliaji (Forwards)
Hakuna shaka kuwa Antonio Di Natale anabaki kuwa legendary kunako klabu hiyo ya Friuri pamoja na serie A kwa ujumla.Atakuwa akiangaliwa kwa kiasi kikubwa katika ushambuliaji.Nguvu imeongezeka katika sehemu hiyo ya ushambuliaji baada ya kuwasili kwa mchezaji anayekuja juu kwa sasa Luis Muriel akitokea kwa mkopo kunako klabu ya Lecce. Uwepo wa Di Natale na Muriel pamoja na viungo washambuliaji kama Maicosuel utaiongezea nguvu klabu ya Udinese katika ushambuliaji na hivyo kukifanya kikosi cha kocha Francesco Guidolin kutikisa msimu ujao.
0 comments:
Post a Comment