
MZUNGUUKO wa pili wa
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara unaanza kesho (Januari 26 mwaka huu) kwa raundi ya 14
ambapo timu 12 kati ya 14 za ligi hiyo zitakuwa uwanjani.
Mabingwa
watetezi Simba watakuwa wenyeji wa African Lyon katika mechi itakayochezwa saa
10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Hiyo itakuwa mechi ya kwanza
kwa kikosi cha Simba tangu kiliporejea kutoka Oman kwenye ziara ya mafunzo.
Mwamuzi
wa kimataifa Israel Mujuni ndiye atakayechezesha mechi hiyo ambapo African Lyon
inatarajiwa kuongozwa na Kocha Charles Otieno baada ya kusitisha kibarua cha
Pablo Velez kutoka Argentina kutokana na kufanya vibaya katika mzunguko wa
kwanza.
Uwanja
wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wenye uwezo wa kumeza watazamaji
8,000 ndiyo utakaohimili vishindo vya mechi kati ya Polisi Morogoro na wenyeji
Mtibwa Sugar. Polisi Morogoro ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa VPL
ililazimisha suluhu katika mechi ya mzunguko wa kwanza.
Coastal
Union ambayo kwenye dirisha dogo imesajili wachezaji sita akiwemo Mzimbabwe
Tinashe Machemedze itaoneshana kazi na wana-Tanga wenzao Mgambo Shooting kwenye
Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Timu
zinazo katikati ya msimamo wa ligi, Ruvu Shooting na JKT Ruvu zitapimana ubavu
kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani ambapo sheria 17
zinazotawala mpira wa miguu zitakuwa chini ya usimamizi wa refa Dominic
Nyamisana kutoka Dodoma.
Wawakilishi
wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam baada ya mechi za
kirafiki nchini Kenya wanarejea kwenye Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuikaribisha
Kagera Sugar ya Kocha Abdallah Kibaden kwenye Uwanja wa Chamazi.
Ni
mechi ya kulipa kisasi kwa Kagera Sugar baada ya kulala bao 1-0 katika mechi ya
mzunguko wa kwanza iliyochezwa Septemba 15 mwaka jana Uwanja wa Kaitaba, mjini
Bukoba.
Maafande
wa Oljoro JKT wanaanza kuchanga upya karata zao katika mzunguko wa pili kwa
kuikaribisha Toto Africans ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh
Kaluta Amri Abeid, jijini Arusha.
0 comments:
Post a Comment