
SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF), limesema Kamati ya
Uchaguzi ya Shirikisho hilo imepanga kukutana kwa mara kwanza kesho Jumatano,
ili kupitia majina yote na pingamizi zilizowekwa kwa wagombea wanaowania nafasi
mbalimbali za uongozi za TFF.
Wagombea ambao wamewekewa pingamizi ni pamoja na
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji, anayewania nafasi ya Bodi ya Ligi, Michael
Wambura, anayetaka nafasi ya Makamu wa Rais, Athuman Nyamlani anayewania Urais,
Jamal Malinzi Urais, sambamba na Mugisha Garibona, Vedastus Lufano wanaowania
nafasi ya Ujumbe, huku wakiwekewa pingamizi na Paul Mhangwa.
Katika taarifa yake iliyotumwa kwenye vyombo vya
habari na Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Angetile Osiah, alisema Kamati ya
Uchaguzi itapitia pingamizi zote zilizowekwa kwa wagombea hao.
Osiah alisema katika kikao hicho cha kujadili
pingamizi kitakachoanza saa nne asubuhi, waombaji wote wa nafasi za uongozi na
wale walioweka pingamizi wanatakiwa kufika katika tukio hilo.
“Wale walioweka pingamizi kwa wagombea na
wanaowania nafasi za uongozi za TFF wote watashiriki kikao hicho cha kujadili
pingamizi,” ilisema taarifa hiyo.
Uchaguzi wa TFF umepangwa kufanyika Februari 24
jijini Dar es Salaam, huku wadau mahiri wa michezo wakipigana vikumbo kuzitaka
nafasi mbalimbali za Shirikisho hilo nchini.
Nafasi zote zimekuwa na ushindani wa aina yake,
huku majina ya wadau kama vile Malinzi, Nyamlani kwa nafasi ya urais, bila
kusahau Manji na Wambura wakipigania ubosi wa TFF katika Uchaguzi wa mwaka
2013.
0 comments:
Post a Comment