MAJOGOO WA JIJI WATAWIKA MSIMU HUU…...?
Kwa kawaida
binadamu akisikia kiu hutafuta maji popote pale yalipo.Na mara maji
yakikosekana ,binadamu huyu hutamani
kunywa chochote kile kilichopo mbele yake ilimradi kiwe ni kimiminika ili
kukata kiu aliyonayo.
Hakika kwa mfano huu wa kiu na maji kwa
binadamu ndivyo navyouona kwa mashabiki wa klabu ya Liverpool ya nchini
Uingereza.Kwani kwa muda mrefu sana mashabiki hawa wamevumilia kiu ya muda
mrefu waliyokuwa nayo ya kutokuwa na vikombe kwa takribani miaka 22 sasa.
Ukibahatika
kumuuliza shabiki yeyote yule wa klabu hii ni kitu gani anachotamani
kukishuhudia katika klabu hiyo ya Liverpool basi hatosita kukwambia kuwa kiu
yake itamalizwa kwa klabu hiyo kuchukua vikombe hasa ubingwa wa ligi kuu wa
nchini Uingereza.
Tangu wachukue ubingwa wa iliyokuwa ligi daraja la kwanza (kwa sasa ligi kuu) nchini Uingereza mwaka 1990, Liverpool bado inahangaika mno kuupata ubingwa wa ligi kuu ya soka wa nchi hiyo.Kwani ni miaka takribani 22 sasa ambapo mashabiki wa Liverpool wamekuwa wakiusikia ubingwa huo wa ligi kuu kwa vilabu vingine kama Manchester United,Chelsea,Arsenal na sasa matajiri wa jiji la Manchester nawazungumzia Manchester City.
Hakika
wapenzi wa kabumbu wataungana nami katika hili kuwa tangu Liverpool wautwae ubingwa
wa iliyokuwa ligi daraja la kwanza(kwa sasa ligi kuu) mwaka 1990, mpaka sasa wanaliverpool
na wapenda kabumbu duniani wameshuhudia vizazi vingi vikipita pasipo kufanikiwa
kuchukua ubingwa wa ligi kuu nchini Uingereza ingawa Liverpool wamekuwa
wakishinda makombe mengine mbali na ligi kuu kama kombe la chama cha mpira wa
miguu nchini Uingereza(kombe la FA),kombe la ligi maarufu kama(Carling Cup) na
klabu bingwa barani ulaya maarufu kama(UEFA Champions League).
Tumepata
kushuhudia vizazi vya wachezaji kama Steven Mc Manaman,Jamie Redknap,Michael
Owen,Robie Fowler,Steven Gerrad mpaka sasa kizazi cha akina Suarez,Joe
Allen,Raheem Sterling ,Pacheco na Jonjo.Vizazi vyote hivyo nilivyotaja,wengi wa
wachezaji waliondoka katika klabu hiyo pasipokuwa na ile medali ya ubingwa wa
ligi kuu ya nchini Uingereza.Hii imezidi kuwafanya mashabiki wa klabu hiyo ya
Anfield kuwa na hamu kubwa sana ya ubingwa huo wa ligi.
Machungu ya
mashabiki hawa pia yanaongezeka katika hali ya kwamba klabu hiyo ya Liverpool
ilichukuliwa kama mabingwa wa kihistoria wa ligi kuu nchini Uingereza kabla ya
mashetani wekundu nawazungumzia Manchester United kuipiku rekodi hiyo ya vijana
hao wa Anfield na hivyo kuzidi kuongeza presha kwa mashabiki wa Merseyside.Liverpool
wameuchukua ubingwa wa ligi ya Uingereza mara 18 wakati Manchester United
wameutwaa ubingwa wa ligi kuu wa nchi hiyo mara 19.
Swali la
kujiuliza ni kuwa,Je ni saa ya ukombozi kwa majogoo hao wa Liverpool chini ya kocha
mpya Brendan Rodgers?
Haya ni
mambo matano(5) ya kiufundi ambayo binafsi tunaweza kuyaona ama kuyashuhudia
kwa klabu ya Liverpool chini ya kocha mpya Brendan Rodgers.
·
Kwanza
timu pinzani zitegemee presha kubwa sana toka katika safu ya ushambuliaji ya
Liverpool.Hiki ndicho nilichokiona msimu uliopita kwa klabu ya Swansea
iliyokuwa na kocha Brendan Rodgers.Washambuliaji wa Swansea Luke Moore,Leroy
Lita na Loveridge walikuwa wakiwasumbua sana mabeki wa timu pinzani kutokana
presha walioipeleka kwa mabeki wa timu hizo pinzani.Presha hii ilionekana kwa
washambuliaji hao kuonekana wakianzia kukaba kwa mbele ili kuwanyima mabeki
nafasi ya kutoa pasi za viungo.Vivyo hivyo nategemea mno kuiona safu ya
ushambuliaji ya akina Luis Suarez,Fabio Borin,Andrew Carol na Pacheco kufanya
hivyo kwa mabeki kama Nemanja Vidic,John Terry,Vicent Kompany,Thomas Vermeleen na
wengine wengi toka vilabu shiriki vya ligi kuu msimu huu ambayo ndiyo falsafa
ya kocha Brendan Rodgers.
·
Tutegemee
soka la pasi na timu kusogea mbele ya lango la wapinzani muda wote.Msimu
uliopita wa (2011-12),klabu ya Swansea ilikuwa ni miongoni mwa vilabu
vilivyoongoza kwa kupiga pasi kwa usahihi ndani ya mchezo katika ardhi ya
Uingereza na nje ya mipaka ya Uingereza sanjari na timu kama Barcelona,Real Madria,Bayern
Munich,Manchester United nk.Jumla ya pasi 2,111 zilipigwa na klabu hiyo huku
pasi 2,107 zikipigwa na viungo wawili bora kabisa kwa sasa nchini Uingereza
ambao ni Leon Briton na Joe Allen.
Takwimu zinaonesha kuwa Leon Briton alipiga pasi sahihi kwa 93% huku
kiungo mwenzake Joe Allen akipiga pasi sahihi 91% katika mechi walizocheza
msimu uliopita.Hakuna hata mchezaji mmoja wa klabu ya Liverpool aliyeweza
kufikisha idadi hiyo ya pasi.Hii ina maana ya kwamba siyo nahodha Steven
Gerrad,Lucas,Charlie Adam wala Jordan Hernderson walioweza kufikisha idadi
kupiga pasi kwa usahihi ya viungo hao.Ila kujiunga kwa mchezaji Joe Allen
kunako klabu hiyo ya Anfield kutaibadiri sura ya sehemu ya kiungo cha Liverpool
katika msimu huu wa ligi ya Uingereza.
·
Tutegemee
pia kasi nzuri katika sehemu za pembeni mwa uwanja(wings).Wakati akiwa na klabu
ya Reading,kocha Brendan Rodgers aliweza kuwatumia mawinga Jimmy Kebbe na Joby
McAnuff ambao waliweza kumsaidia katika falsafa yake ya kuhakikisha kuwa
mawinga wanatumika katika mashambulizi ya klabu hiyo ya Reading.Akiwa na
Swansea aliweza kuwapika vizuri mawinga Scott Sinclair,Nathan Dyer na Wayne
Routledge katika kushambulia mabeki wa timu pinzani.
Liverpool hawakuwa na mawinga wenye kasi wa kariba ya Sinclair,Dyer na
Routledge na hivyo kwa kiasi kikubwa kulidhoofisha sehemu ya ushambuliaji ya
klabu hiyo ya Anfield kwani ni Luis Suarez pekee aliyekuwa katika fomu ya hali
ya juu sana hasa wakati ambapo alikuwa akitokea pembeni kuingia ndani ya eneo
la timu pinzani.Hivyo ujio wa Brendan Rodgers utaifufua sehenu hiyo ya pembeni
ya Liverpool ikizingatiwa kuwa kuna uwepo wa mawinga asilia kama Stewart
Downing,Rahim Sterling, na Joe Cole.
·
Liverpool
hawatotegemea sana mashambulizi ya kushtukiza msimu huu kwa maana ya(counter
attack) huku msisitizo ukiwa kushambulia kuanzia sehemu ya ulinzi.
Ukiwaangalia vizuri Swansea msimu uliopita,utagundua kuwa timu yao
ilijengeka vizuri sana kimashambulizi kuanzia sehemu ya mabeki halafu viungo na
mwisho ni washambuliaji.Mabeki kama nahodha Gary Monk,nahodha msaidizi Alan
Tate,Chico na bila kumsahau Ashley Williams walikuwa wazuri katika kuanzisha
mashambulizi ambayo yalipokelewa vizuri na viungo kama Joe Allen(amehamia
Liverpool),Leon Briton,Scott Sinclair mpaka kwa washambuliaji Leroy Lita na
Luke Moore.
Mfumo huo huo wa mashambulizi tunatarajia kuuona katika klabu ya
Liverpool ambapo mabeki Daniel Agger,Sebastian Coates,Martin Sktel,Glen Johnson
na wengineo wakianzisha mashambulizi na si kuwategemea kina Gerrard,Joe Allen,Charlie
Adam na Luis Suarez pekee katika kuanzisha mashamulizi.
·
Tutegemee
kuimarika kwa safu ya ushambuliaji kutokana na
kusajiliwa wachezaji wapya ili kusaidiana na Luis Suarez.
Sehemu ya ushambuliaji iliwaangusha sana Liverpool msimu uliopita.Katika
sehemu hiyo ya ushambuliaji ni mchezaji mmoja tu aliyekuwa katika fomu ya hali
ya juu sana pamoja na kukumbwa na rungu la chama cha soka nchini Uingereza(FA)
la kufungiwa mechi nane(8) kutokana na kashfa ya ubaguzi kwa mchezaji wa
Manchester United Patrice Evra namzungumzia Luis Suarez.Hakika Suarez alikuwa
na mchango mkubwa sana kwa klabu hiyo ya Anfield msimu uliopita.Aliweza
kuwazidi washambuliaji wengine kama Andrew Carol,Craig Bellamy na Dirk Kuyt.
- Suarez ndiye alikuwa mfungaji bora wa Liverpool msimu uliopita akifunga
magoli kumi na moja (11).
- Suarez alishika nafasi ya pili kwa kupiga pasi za magoli kwa Liverpool
nyuma ya kiungo Charlie Adam.Charlie alitoa pasi sita (6) za magoli wakati
Suarez alitoa pasi (3) za magoli.
- Suarez aliongoza kwa kupiga mashuti langoni mwa timu pinzani huku
akipiga mashuti 128 kati ya hayo mashuti 48 yakilenga goli.Bila kusahau kuwa
Suarez ndiye mchezaji aliyefanyiwa madhambi(faulo) kuliko mchezaji yeyote pale
Liverpool akifanyiwa faulo mara 74.
Kwa ujumla
sehemu ya ushambuliaji katika klabu ya Liverpool ilimhitaji mchezaji atakayesaidiana
na Luis Suarez hasa katika eneo la theluthi ya mwisho ya eneo la wapinzani
maarufu kama(final third).Hivyo ujio wa Fabio Borini,uwepo wa Andrew Carol na
makinda kama Pacheco na Raheem Sterling utampunguzia Suarez kwa kiasi kikubwa
mzigo aliokuwa nao msimu uliopita pale Anfield.Hata hivyo usajiri bado
unaendelea na hivyo tunaweza kushuhudia majina mengine yakitua pale Anfield.
Hivyo ndivyo navyoitazama Liverpool chini ya kocha Brendan Rodgers kwa
msimu mpya wa 2012-13.
KILA LA KHERI LIVERPOOL KATIKA MSIMU HUU MPYA WA LIGI KUU YA SOKA NCHINI
UINGEREZA
0 comments:
Post a Comment