Quintel Blogger theme

A free Premium Blogger theme from newbloggerthemes.com

Sunday, October 7, 2012

EL CLASSICO NI ZAIDI YA PAMBANO


Hakika ni jumapili nzuri sana leo kwa ndugu zangu wapenda kandanda kwani baada ya kutoka katika nyumba za ibada kwa wale wakristu na kwa waislamu najua ibada pia zinaendelea kama kawaida watu watakuwa wapo majumbani wakisubiria kwa hamu mechi za leo.Leo naweza kuiita ni ‘Super Sunday’kwani kuna takribani mechi 3 mpaka 4 za kuzitazama likiwemo pambano la kukata na shoka kati ya Fc Barcelona na Real Madrid katika dimba la Camp Nou pale nchini Hispania.

Kwa wale mashabiki wa Ligi Kuu ya soka nchini Italia watapata kulishuhudia pambano la kukata na shoka kati ya AC Milan dhidi ya Inter Milan pambano likijulikana kama ‘Derby Della Madoninna’.Lakini kwa leo ningependa nilizungumzie zaidi pambano la watani wa jadi nchini Hispania maarufu kama ‘EL CLASSICO kati ya Barcelona dhidi ya Real Madrid’.
Watu wengi wanajiuliza kwa nini pambano hili linaitwa ‘EL Classico’.Jina la EL Classico halikuanza zamani sana kwani lilianza katika miaka ya 2000.Asili yake ni katika nchi za Amerika ya Kusini kutokana na kuongezeka nguvu kwa soka la Hispania katika bara hilo la Amerika.Nchini Argentina pambano la wapinzani wa jadi kati ya Boca Juniors na River Plate linajulikana kama Superclassico,wakati nchini Mexico pambano la watani kati ya Club America na Guadalajara linajulikana kama El Super Clasico.
Kabla hata ya jina hilo la El Classico nchini Hispania,tayari mashabiki wa soka wa Hispania walishaonja utamu wa upinzani wa jadi baina ya timu hizo tangu mwanzoni mwa karne ya 20.Na moja ya sababu ya upinzani huu ni kuwa timu zote mbili zimetoka katika majiji makubwa mawili nchini Hispania ya Madrid na Catalunya.

Inasemekana kuwa klabu ya Real Madrid inapendwa sana na viongozi wakubwa wa serikali pamoja na familia ya kifalme ya nchini  Hispania huku watu wa jimbo la Catalunya ambapo klabu ya Barcelona ndipo inapotoka inawakilishwa na watu wa kawaida na wenye kipato cha kawaida.Upinzani wa vilabu hivi ulikolezwa zaidi na nguli wa soka duniani Alfredo Di Stefano ambaye amepewa cheo cha Rais wa Maisha wa klabu ya Real Madrid katika miaka ya 1950 wakati klabu zote mbili za Madrid na Bracelona zikiingia katika mgogoro wa kumsajili nyota huyo aliyekuwa akikipiga katika klabu ya Derpotivo  Los Milonarios ya nchini Colombia.

Di Sefano alivitoa udenda vilabu vya Real Madrid na Barcelona wakati akiichezea klabu ya Deportivo Los Milonarios ya Bogota nchini Colombia.Alivyotoka Depo ya nchini Colombia alijiunga na klabu ya River Plate ya nchini Argentina kabla ya vilabu vya Barca na Madrid kila moja kumsajili na hivyo kuibua mgogoro mkubwa wa kuwa ni klabu gani ilipaswa kupata sahihi ya mchezaji huyo.Mgogoro huo uliingiliwa kati na chama cha soka cha nchini Hispania na kumuidhinisha Di Stefano kuichezea klabu ya Real Madrid na Barcelona ikipigwa chini.

Katika kuonesha yeye ni mchezaji hatari,Di Stefano alifunga magoli mawili mazuri katika pambano la wapinzani hao wa jadi katika mechi yake ya kwanza dhidi ya timu ya Barcelona wakati akiwa na jezi za Real Madrid.Upinzani wa jadi wa vilabu hivi uliongezeka maradufu wakati timu hizo zilipokutana mara mbili katika michuano ya Ulaya kati miaka ya 1960 na 1961.Mwaka 1960 Real Madrid iliifunga klabu ya Barcelona katika fainali ya michuano hiyo ya Ulaya kwa sasa klabu bingwa Ulaya  na mwaka 1961 Barcelona ilifanya vivyo hivyo.

Sababu nyingine ya mechi hii kuwa na mvuto ni kitendo cha wachezaji nyota kuvichezea vilabu hivi viwili katika nyakati tofauti.Wengi watakumbuka mwaka 1980 ambapo wachezaji nyota Bernd Schuster alipoikacha Barcelona na kujiunga na Real Madrid huku  Michael Laudrup ambaye kwa sasa anaifundisha klabu ya Swansea City ya nchini Uingereza akifanya hivyo mwaka 1990.

Mwaka 2000 Luis Figo akifanya vivyo hivyo kwa kuikacha Barcelona na kujiunga na klabu ya Real Madrid.Pambano la kwanza baina ya timu hizi mbili lilifanyika tarehe 17 mwezi wa pili(Februari) mwaka 1929 pale Camp Nou huku Madrid ikiibuka na ushindi wa magoli 2-1.Wakati uhamisho wa wachezaji kama Luis Enrique kutoka Real madrid kwenda Barcelona na Luis Figo kutoka Barcelona kwenda Real madrid ukizua vurugu kubwa lakini upinzani wa vilabu hivyo haujavizuia vilabu hivyo kuuziana wachezaji.

Wachezaji Ricardo Zamora,Josep Samitier,Bernd Schuster,Michael Laudrup na Ronaldo Di Lima wote wamewahi kuvichezea vilabu hivi kwa nyakati tofauti.

Mechi ya Leo.

Pambano la leo kati ya Barcelona na Real Madrid linasubiriwa kwa hamu sana na wapenda kabumbu takribani 400 duniani litakuwa la kukata na shoka.Barcelona wataingia uwanjani huku wakiwa na listi ya majeruhi kama nahodha Carles Puyol aliyevunjika mkono,Thiago Alcantara na kukiwa na hatihati kwa beki wake tegemeo Gerad Pique kuwemo katika kikosi.Tayari viungo Alex Song na Javier mascherano wametayarishwa kucheza ktika nafasi za mabeki wa kati kwa upande wa Barca.

Kwa Upande wa Real Madrid mtihani mkubwa kwa kocha Mourinho utakuwa ni nani atacheza kama kiungo mshambuliaji katika mechi ya leo kati ya Mesut Ozil,Luka Modric na Ricardo Kaka.Na kati ya Essien na Sami Khedira nani kuanza sambamba na Xabi Alonso katika kiungo.

 TAKWIMU.
·         Leo ni mechi ya 222 kati ya wapinzani hawa wa jadi na kati ya hizo barcelona kashinda mara 87 huku Real akishinda mara 88.
·         Ronaldo kafunga magoli 12 katika mashindano yote magoli 2 mbele ya Lionel Messi mwenye magoli 10.
·         Real Mdrid imeshinda mara moja tu katika mechi 8 ilizocheza Camp Nou chini ya Mourinho huku ikitoka sare mechi 1 na kupoteza 6.

VIKOSI TARAJIWA.
BARCELONA                                                                              
Valdes
Alves, Song, Mascherano, Adriano
Xavi, Busquets, Iniesta
Pedro, Messi, Sanchez                                                         

REAL MADRID
Casillas
Arbeloa, Pepe, Ramos, Marcelo
Khedira, Alonso
Di Maria, Ozil, Ronaldo
Benzema


0 comments:

Post a Comment