
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja
kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini Jumapili (Februari 3 mwaka huu)
kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon (Indomitable Lions).
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam
leo (Januari 31 mwaka huu), Kim amesema mechi dhidi ya Cameroon itakuwa kipimo
kizuri kwake kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya kucheza mechi ya
mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayofanyika Machi mwaka huu.
“Itakuwa mechi ngumu na kipimo sahihi kwetu. Tuko
tayari, tutacheza kwa staili yetu kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya
mechi dhidi ya Morocco. Ni mechi nzuri kwa sababu wachezaji wameonyesha wako
tayari.
“Tumetoka kucheza dhidi ya Zambia na Ethiopia.
Lengo ni Taifa Stars kucheza fainali za AFCON 2015, kwa hiyo mechi dhidi ya
Cameroon ni sehemu ya mipango yetu kuhakikisha tunafika huko,” amesema Kim
ambaye amerejea nchini juzi kutoka Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Morocco
na Ivory Coast zilizo kundi moja na Tanzania katika mechi za mchujo za Kombe la
Dunia.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Stars inashika nafasi ya pili katika kundi lake nyuma ya Ivory Coast
inayoongoza. Timu nyingine katika kundi hilo ni Gambia.
Wachezaji aliowaita kwenye kikosi chake ni makipa
Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam).
Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo
(Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga),
Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Simon Msuva (Yanga),
Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam),
Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba).
Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na Mbwana
Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Katika kikosi hiki, Poulsen hajamuita Jerry Tegete
ambaye siku za karibuni amefufua makali yake wakati ameita washambuliaji halisi
wawili tu, Ulimwengu na Samatta.
Nyota wa timu ya taifa ya Cameroon wanaotarajiwa kuja ni pamoja na:
Charles Itandje, Mayebi Joslain, Allan Nyom, Benedict Angbwa, Benoît
Assou Ekotto, Henri Bedimo, Nicolas Nkoulou, Jean Armel Kana Biyick,
Bouba Aminou, Joel Matip, Alexandre Song, Nguemo Landry, Pierre Wome
Nlend, Hervé Tchami, Fabrice Olinga Essono, Achille Emana, Eloundou
Charles, Jean Makoun II, Samuel Eto'o Fils, Vincent Aboubakar, Jean Paul
Yontcha
0 comments:
Post a Comment